WAKUU wa shule za sekondari nchini wametakiwa kuacha tabia ya
kusajili wanafunzi ambao hawajapata nafasi ya kuchaguliwa kujiunga na
elimu ya sekondari, kwa kigezo cha kuziba nafasi ya wale waliochaguliwa
na kushindwa kuripoti kwa muda mwafaka.
Badala yake wafuate taratibu na kanuni za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi katika kusaili wanafunzi.
Viongozi hao waliopewa dhamana ya kusimamia taratibu za kuhakiki
wanafunzi wanaojiunga na elimu hiyo, walipewa onyo hilo juzi mjini
Kibaha, katika mkutano wa wa Umoja wa Wakuu wa Shule za Sekondari
Tanzania.
Onyo hilo lilitolewa na Mwakilishi wa Mkaguzi Mkuu wa Shule za
Sekondari katika Kanda ya Mashariki, Paulo Moshi, ambaye alisema vitendo
hivyo vinapingana na sheria za nchi.
Alisema kuwa kitendo cha baadhi ya wakuu wa shule za sekondari
kuwasajili kinyemela wanafunzi ambao hawakuchaguliwa, kinarudisha nyuma
maendeleo ya elimu.
Alisema hiyo inatokana na ukweli kwamba baadhi ya wanafunzi hao
wanakuwa wanaingia katika shule za sekondari, huku wakiwa hawana sifa
inayostahiki.
“Napenda kuwasihi juu ya hili kuwa hiki ni kitendo ambacho
kinarudisha nyuma maendeleo ya nchi hasa katika nyanja ya elimu, naomba
tujirekebishe kama kutakuwa na wanafunzi wanaoshindwa kuripoti kwa muda
mwafaka kwa sababu mbalimbali, basi tutumie kanuni zetu zilizowekwa na
Wizara ya Elimu,”alisema Moshi.
No comments:
Post a Comment