FATMA binti Baraka, maarufu kwa jina la Bi Kidude, ni miongoni mwa
wasanii wanawake wachache ambao ni magwiji wa muziki wa taarabu nchini,
ambaye kwa siku ya leo ataibeba manowari yetu ya Siku ya Wanawake
Duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka ifikapo Machi 8.
Bibi huyu mwenye sauti nzito na inayopenya vyema masikioni mara
anapoimba, ni mzaliwa wa Zanzibar lakini asili ya kabila lake ni
Mmanyema kutoka Mkoa wa Kigoma, magharibi mwa nchi.
Licha ya kuwa na umri mkubwa (113) , sauti ya Bi Kidude bado ni nzuri
na yenye kuvuta hisia, hasa kwa mpenzi wa miondoko ya muziki wa mwambao.
Bi Kidude katika nyimbo zake nyingi amekuwa akiwavutia wengi kutokana
na nyimbo zake kubeba ujumbe wa mahaba kama alivyoimba kwenye wimbo wake
’Ya Laiti napenda pasi kifani’ na wakati mwingine mafumbo kwa lugha ya
Kiswahili yenye lengo la kufikisha ujumbe kwa watu maalumu kama
alivyoimba katika wimbo wake wa ’Muhogo wa Jang’ombe’.
Hadi hapo utaona kwamba mtu mzima huyu anapaswa kupewa heshima katika
siku kama hii, hasa kwa kuzingatia kwamba ni Siku ya Wanawake Duniani.
Historia na asili ya jina Kidude
Fatma Baraka kwa kauli yake, anasema amezaliwa miaka 113 iliyopita
huko Zanzibar ambako baba yake mzazi alilowea akitokea Kigoma (enzi za
utumwa), hivyo kabila lake ni Mmanyema, tena mwenyewe anajiita ni
Mmanyema asilia.
Ingawa hafahamu kijiji halisi alichozaliwa baba yake,
Bi kidude anasema babu yake upande wa mama alikuwa Mngindo, wenyeji wa Kilwa.
“Mimi asili yangu ni Mmanyema wa Kigoma, baba yangu na mama yangu
alikuwa Mngindo, lakini baba yangu alilowea Zanzibar, ndiyo nasisi
tukazaliwa huko mpaka sasa naishi Zanzibar, lakini mie Mmanyema,”
anasema Bi kidude alipozungumza na Tanzania Daima hivi karibuni.
Anasema jina la Kidude alipewa na mjomba wake wakati alipozaliwa kwa
sababu alikuwa na umbile dogo. “Nimezaliwa miezi saba... njiti,
nililazwa kitandani, nilikuwa mdogo, mtu hawezi kujua kama kuna kitu
kimelazwa.
“Kuna mjomba wangu akaja akakaa nilipolazwa mimi, akaambiwa angalia
usimkalie mtoto, akasema mtoto gani, ni kidude tu hiki, basi ndo tangu
siku hiyo jina limenieleleza.
Mkongwe huyu wa taarabu nchini, ambaye kwa miaka ya hivi karibuni
amejizolea umaarufu kupitia tasnia hiyo, anasema katika maisha yake
hajapata kuwa na mtoto, ingawa ameweka bayana kwamba aliwahi kuolewa
mara mbili.
Kwa muonekano ni kikongwe mwenye nguvu zake, anasema katika umri
alionao, amepitia misukosuko ya aina tofauti za maisha. Kifupi, safari
yake kimaisha ni ndefu.
Anafafanua kwamba ndoa yake ya kwanza alifunga na Ramadhani Ibrahimu, na wa pili aliitwa Juma Kombo.
“Nimeolewa vyuo viwili, cha kwanza nikaachika, nimewahi kumfumania
mume wangu (nadhani anamaanisha huyo wa pili), nikampiga kwa mikia ya
taa nikamwacha anachuruzika damu, nikaenda zangu na mpaka leo sijaolewa
na wala sina haja ya kuwa na mume,” anasema.
“Sijisifu, ila miye mpaka kesho ukiniudhi wallahi sitafuti mtu...
nitawatuma watu wakuite, ukifika mie nimeandaa fimbo yangu, nikikuchapa
nayo, ikimpata mtu anasimama kama anatafuta pesa,” anasema Bi kidude na
kuongeza utani, jambo linalokulazimu kuendelea kumsikiliza bila kuchoka.
Anaendelea kuwausia hususan wasichana walio katika umri wa kuolewa
kwamba wanaume wa sasa hivi si wema wengi wanapenda kumkuta mwanamke ana
kila kitu. “Hakuna wanaume sasa hivi, hao walikuwepo zamani, siyo
leo... leo mwanaume anakufuata, umlishe, umfanyie kila kitu, waapiii!
Wanaume enzi hizo,” anasisitiza Bi kidude.
Maisha yake na uimbaji
Mkongwe huyu wa taarabu na muziki wa mwambao nchini anainadi siri yake
katika fani kuwa ni kipaji. Katika hilo Bi Kidude anasema ameanza
kuimba akiwa binti wa miaka 10, alipokuwa akitoroka kwao na kwenda
nyumbani kwa marehemu Mtumwa binti Saadi, maarufu Siti binti Saad.
Kadhalika, anatanabaisha kwamba mafanikio kwa mwanamuziki bora ni yule
anayetumia kichwa na dhati ya moyo wake kwenye kuimba. Anasema kubana
au kuibadili sauti wakati wa kuimba si sahihi, inamtoa mwimbaji kwenye
uhalisia wake.
“Mie naimba kwa kutumia kichwa, si kifua au kubana pua aaa! Sifanyi
kama hao wanaojiita waimba taarabu wa siku hizi, kwanza siku hizi hakuna
taarabu. Mimi nina uwezo wa kuimba bila kutumia karatasi... kwani bendi
ya polisi! (kicheko kwa wanaomsikiliza).
“Enzi zetu taarabu ulikuwa mtu ukiisikiliza ufanye kazi kupata maana
yake kutaka kulinda matusi na kila mmoja anaweza kuisikiliza popote.
Kwanza watu walikuwa wanaanza kuimba saa nane za usiku, ikifika saa 11
unafungwa muziki. Mie nashangaa siku hizi taarabu inaanza saa mbili.
“Taarabu ya zamani mtu ulikuwa ukitisa kichwa taratibu, wanawake
tulikuwa tunavaa kwa heshima, si siku hizi watu mnakatika mabuno
(viuno), wanawake wanakwenda bila heshima, au kwa vile kuna matako ya
Kichina?” anahoji mwanamuziki huyo huku akitoa pakiti yake ya sigara
aina ya Embassy na kuvuta.
Kuhusu sigara na uimbaji, Bi kidude hakubaliani na dhana kwamba
inamaliza sauti, badala yake anashuhudia kwamba ameanza kuvuta akiwa
kijana lakini sauti yake haina mabadiliko.
“Nimevuta sigara mie hujazaliwa na mpaka sasa navuta sijapata TB wala
ugonjwa wa mapafu, leo unaniambia mbaya! Mbona sijafa?” anahoji mkongwe
huyo na kueleza kwamba alianza kuvuta sigara aina ya Seven Seven, Mkasi,
Simba, Kulindondo, Gundufleki na sasa Embassy ambapo ana uwezo wa
kumaliza pakiti moja kwa siku tatu.
Mbali ya kuimba, pia Bi kidude ana uwezo wa kupiga ngoma, ikiwa ni
baada ya kujifunza kwenye majahazi wakati akiwa na umri mdogo alipokuwa
akitoroka kwenda madrasa (chuo cha elimu ya Kiislamu).
“Nilikuwa nakimbia nyumbani, naaga naenda chuo lakini sifiki, nazuga
kwa kubeba juzuu yangu kwapani lakini siendi huko, bali nakwenda kwenye
majahazi kufundishwa kupiga ngoma na tumba,” anasisitiza.
Oktoba mwaka 2005 alipata Tuzo ya heshima ya msanii mwenye mafanikio makubwa iliyotolewa nchini Uingereza (tuzo ya WOMAX).
Aliyebaini kipaji chake
Bi Kidude, anapasua ukweli kwamba mtu wa kwanza kuthamini kazi zake na
kumtafuta hadi kufika alipo alikuwa Rais mstaafu wa Tanzania wa Awamu
ya Pili, Ali Hassan Mwinyi.
Anasema alipokuwa Rais wa Zanzibar, aliwaomba watu wamtafute Bi Kidude
ili apate kumwimbia nyimbo za Siti, kwa kuwa hakuna aliyeweza kuziba
pengo japo kidogo la Siti binti Saad.
“Ali Mwinyi alikuwa akitafuta nyimbo za Siti binti Saad. Akatumwa Vuai na Khadija Baramia ambao siku nyingi hatujaonana.
“Walipotokea wakaniambia natafutwa na Ali Hassan Mwinyi, mie
nikashangaa, kwa sababu nyumba zetu zilikuwa zikitizamana milango,
nikaona bora niende... nikapelekwa Bwawani nikatengenezewa chumba kama
kuku.
“Teena! Nikawa namwimbia Mwinyi kule Bwawani akija anaburudika... huko
nikakutana na Mariam Hamdani (dada wa aliyekuwa Waziri wa Fedha, Zakhia
Hamdani Meghji) alikuwa anakuja kunipiga picha anapeleka Ujerumani miye
Bi Kidude sijui,” anasema.
Aidha, anafahamisha kwamba alipelekwa kwa mara ya kwanza nchini
Ujerumani na Mariam Hamdani, aliyemtambulisha kwa watu mbalimbali ambapo
aliweza kusimama kwenye majukwaa na kutumbuiza.
Kama hiyo haitoshi, Bi kidude anaongeza kwa kusema Mariam alimpeleka
hadi kwa Malkia Elizabeth II nchini Uingereza. “Yeye ndiye alinipeleka
Ulaya, sikujua Kiingereza, nikawa na mlinzi, miye nimefika hadi kwa
Malkia Mtukufu Lizabet (Elizabeth)... akawa ananisalimia Shikamoo mama
Kidude.
“Nimepewa cheo na Mtukufu Lizabet. Nilipofika anafunua vitabu naona
sura yangu nikawa nashangaa, alinipa kidani cha dhahabu nikaamua kukiuza
kulekule Uingereza, maana ningekuja nacho huku wangeniua,” anasema.
Katika hilo, Bi kidude anasema alipofika kwenye kasri la malkia
alikutana na askari waliofanana na sanamu, wamevalia viatu vya chuma
huku akieleza kwamba hajawahi kuliona kochi kama aliloliona huko.
“Wakati natoka kwa Mtukufu Lizabet nilijikojolea ndani ya gari kwa
hofu mambo niliyoyaona makubwa,” anasema Bi Kidude ambaye ni binamu wa
aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Salmin Amour.
Akiwa nje ya Tanzania, mkongwe huyo anaeleza anavyothaminiwa huku
akisisitiza kwamba Mkurugenzi wa Nyumba ya Vipaji Tanzania (THT), Ruge
Mutahaba, pia alimsaidia na kumfikisha alipo.
“Mimi, Ruge miye sikumjua huku, kanikuta napiga ngoma kwa Shakira,
kanipenda akanichukua kaenda kunikodia hoteli alipojua naimba ndo
akanikaribisha ofisini kwake, tunaongea ananihoji, kisha ananipa pesa
anaondoka, mie nabaki hotelini tena.
“Siwi na shida miye, nakwenda ofisini kwa Ruge, simuombi mwenyewe
ananigawia pesa, ananiuliza upo au haupo, namwambia narudi Unguja na
yeye akija Unguja lazima afike nyumbani kwangu, anachukua alichonacho
ananigawia, simuombi aah! Ananitumikia yeye. Hii ni mara ya pili anakuja
kunichukua kwa ajili ya tamasha,” anasisitiza huku akimwomba Mungu
ambariki mkurugenzi huyo.
Miongoni mwa nyimbo zinazompa umaarufu Bi kidude hadi sasa ni Muhogo
wa Jang’ombe, Yalaiti, Kijiti, Arebaba na Machozi, Machozi ya huba na
nyinginezo.
Anavyoijua Dar es Salaam
Bi kidude anasema anaifahamu vilivyo Dar es Salaam kwa kuwa amefika
hapa enzi za utawala wa Mwarabu wakati wazawa wakitoa kodi ya kichwa.
“Nchii hii kaitengeneza John Rupia miye niko hapa, mama Haambiliki
alikuwa anafanya vichekesho, nimemlea miye, mama mzazi wa mwanamuziki
Shakira nimemlea miye. Hao kina Mzee Yusuf nimewalea wazazi wao.
“Nimekuja hapa binti sijaolewa, nimekuja kwa madhumuni ya kuimba
taarabu, nilifikia Bagamoyo, Rais Jakaya Kikwete, kazaliwa mikononi
mwangu mie, nilikuwa naishi kwa Sheikh Ramia.
“Nimewahi kuishi Ajipshini (Egyptian) kwa miaka tisa,” anasisitiza
gwiji huyo wa miondoko ya taarabu ambaye hivi karibuni alikonga nafsi ya
Rais Kikwete na Watanzania waliohudhuria uzinduzi wa kampeni ya Mradi
wa Malaria iliyokwenda kwa jina la ’Zinduka.’
Pages
Search This Blog
ushauri
Fay Pub
tangaza
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment