RAIS
mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi amerejea kauli yake kuhusu
mgogoro wa udini akisema kila mtu ana haki ya kuchinja kutokana na imani
yake ilimradi tu asivunje sheria za nchi.
Mwinyi alisema anashangaa kuona watu wakigombania kitu kidogo kama kuchinja ilihali Tanzania ina utamaduni wa amani siku zote na kwamba kila mtu ana imani yake ya dini anayoiamini.
Kiongozi huyo mstaafu alitoa msimamo huo jana jijini Dar es Salaam katika kongamano juu ya utamaduni wa Kiislamu Afrika Mashariki ambapo Tanzania imechaguliwa kuwa mwenyeji.
“Imani ni nafsi ya mtu na haitakiwi kumlazimisha kula nyama iliyochinjwa na mwenzie. Na kama unaona aliyochinja mwenzio ni kibudu basi usile chinja yako, kula hata ukitaka kula chura, mjusi, konokono, kula utakacho ruksa ilimradi tu usiingie katika jinai,” alisema.
Mwinyi alikumbusha kuwa hata wakati wa utawala wake majaribu kama hayo yaliwahi kumtokea, lakini alijitahidi kuweka sawa kwa kumwambia kila mtu ale kile anachofikiri ni chakula bila kumlazimisha mwenzake.
Alisema Watanzania wamezaliwa ardhi moja na kwamba kinachotakiwa ni kuwa na misingi ya kuvumiliana, na kwamba sifa ya Uislamu ni pamoja na kuwa na uvumilivu.
Aliongeza kuwa Uislamu si kufanya vurugu kama inayotafsiriwa na makundi ya wanaotaka kuvunja amani ya nchi kwa kutumia jina la dini ya Kiislamu.
No comments:
Post a Comment