KAMPUNI ya Push Mobile Limited imeahidi kuboresha kazi za
wanamuziki pamoja na asilimia ya malipo yanayotokana na milio na miito
ya simu.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni
hiyo, Freddie Manento katika mkutano na wanamuziki na wadau wa muziki
uliofanyika kwenye hotel ya Serena.
Manento alisema hayo
baada ya kuweka bayana mchakato mzima wa mfumo wa biashara ya muziki
Tanzania katika mkutano uliohudhuria na wasanii zaidi ya 80 wa muziki wa
aina tofauti ikiwa kama injili, bongo fleva, muziki wa dansi, taarab na
reggae, hip hop na watayarishaji mbali mbali (producers).
Alisema kuwa kwa sasa Push Mobile inatoa wastani wa asilimia 20 mpaka
40 kwa mwanamuziki pamoja na wadau wao . Alisema kuwa kiwango hicho
hutolewa baada ya wao kupokea kutoka kwa mitandao ya simu kati ya
asilimia 35 mpaka 60.
“Lengo letu ni kuona wanamuziki
wanafaidika na kazi zao hasa kupitia milio na miito ya simu, biashara
ambayo kwa sasa imewaingizia kipato kikubwa wanamuziki baada ya kuanguka
kwa soko la mauzo ya albamu e na kutopata kipato chochote kutoka kwenye
redio na televisheni kama ilivyoelezwa na Naibu Waziri wa Mawasiliano ,
Sayansi na Teknolojia wakati anajibu hoja ya Mbunge wa Chadema, Zitto
Kabwe,” alisema Manento.
Alisema kuwa asilimia ngapi
wataongeza, itatokana na majadiliano na kampuni za mitandao ya simu na
hata kama kampuni hizo zitakataa kuongeza ili kuwafaidisha wasanii, wao
wataongeza tu.
Alifafanua kuwa kampuni yao imekuwa
ikiingia gharama kubwa za kiuendeshaji katika kupromoti nyimbo za
wasanii ili kuweza kupata soko.
“Tunatumia si chini ya
milioni 25 kwa mwezi kwa ajili ya kuandaa matangazo na kudhamini vipindi
katika redio na televisheni kwa ajili ya kupromoti nyimbo za wasanii
ili kuweza kupata masoko, pia tunatumia zaidi ya million 7 kwa kazi ya
kutengeneza nyimbo ili ziwezwe kuingizwa katika mifumo mbali mbali ya
simu za mikononi,” alisema.
Kuhusiana na kuchelewa kwa
malipo ya wanamuziki, Manento alisema kuwa tatizo hilo linatokana na
ucheleweshwaji wa wadau husika kufanya malipo kwa wakati.
“Push imejitahidi kuondoa tatizo hilo kwa kuwalipa wanamuziki kwa fedha
zake huku ikiendelea kudai kutoka kwa wadau husika ambao mara nyingine
ukaa miezi sita bila kutulipa, ni changamoto kwetu, lakini tumejitahidi
kufikia malengo na kutatua matatizo kwa wasanii, japo changamoto ni
kubwa, nawaomba wanamuziki kuelewa tatizo hilo, ” alisema.
Akizungumza katika mkutano huo mtayarishaji maarufu wa muziki nchini,
John Water Sharizo au Man Water aliipongeza Push Mobile kwa jitihada
zake za kuinua kipato kwa wanamuziki kwani zamani walikuwa wananyonywa
sana katika mauzo ya albamu.
Man Water alisema kuwa ni
jukumu la Push Mobile ambayo inafanya kazi na wanamuziki wengi hapa
nchini kuhakikisha kuwa wateja wake wanapata faida na kazi zao kwani wao
ndiyo wameingia mikataba na wanamuziki na wala siyo makampuni ya simu.
Alisema kuwa wanashukuru kwa kipato kilichopo kwani hapo awali walikuwa
wanachapisha CD au kaseti 200 na kuuzwa mwaka mzima bila kupata mrahaba
kinyume na sasa.
Wanamuziki mbali mbali walihudhuria
mkutano huo walifuraishwa sana kwani waliweza kuweka hadharani kero zao
mbali mbali na kujibiwa na mkurugenzi huyo na kuridhishwa.
Pages
Search This Blog
ushauri
Fay Pub
tangaza
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment